TCAA YASHIRIKI KONGAMANO LA KWANZA LA TEKNOLOJIA YA NDEGE NYUKI NA NDEGE KWA UJUMLA
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Bw. Ludovick Nduhiye amefungua Kongamano la kwanza la Teknolojia ya Ndege Nyuki pamoja na Ndege kwa ujumla kati ya Ujerumani na Tanzania lililofanyika katika Hoteli ya Four Points by Sheraton Novemba 18, 2024, jijini Dar es Salaam.
Katika ufunguzi huo, Bw Nduhiye amesema Serikali ya Tanzania imejizatiti kuhakikisha kunakuwa na usalama na udhibiti mzuri wa teknolojia hizo kwa sababu ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi. Na amewahimiza waendeshaji na washika dau wote kuchukua hatua za kuhakikisha kunakuwa na uaminifu wa viwango vya kimataifa katika kuzuia uingizwaji wowote usio halali.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Daniel Malanga katika wasilisho lake kuhusu TCAA na ameelezea majukumu na kazi mbalimbali zinazozifanywa ikiwemo eneo la udhibiti wa usalama wa ndege nyuki nchini.
Mada nyingine imegusia kuhusu taratibu za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya muingizaji wa ndege nyuki nchini bila kibali ambapo Mkaguzi wa Ndege Nyuki kutoka TCAA, Bw. Ibrahim Abdallah amesema, kwa mujibu wa sheria ya nchi ya udhibiti wa ndege nyuki, mtu yeyote haruhusiwi kutumia ndege nyuki ikiwa haijasajiliwa na Mamlaka, vilevile ndege nyuki zinazoingia nchini zinatakiwa zipatiwe kibali cha kuingia kabla ya kufika nchini.
Mkaguzi Abdalah ameelezea pia juu ya fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo kwenye ndege nyuki, katika eneo la kilimo, madini, kupambana na majangili, kupambana na wanyama waharibifu, kudhibiti uvuvi haramu na kusambaza madawa katika maeneo yasiofikika kutokana na changamoto za barabara.
Kongamano hilo limeandaliwa na taasisi ya AHK Services Eastern Africa Limited kutoka Ujerumani, lengo likiwa kuwaleta pamoja wadau wakuu kutoka Tanzania na Ujerumani ili kuimarisha na kutoa fursa katika teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani.